Katika sura ya pili ya kitabu cha Mwanzo tunaona Muumba akimzawadia mwanamume wa kwanza kwa mpenzi wake. Kisha bwana arusi anapagawa mbele za Mungu akisema, “huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu” (Mwanzo 2:23). Alikuwa pekee na mpweke katikati ya umati. Sasa amempata wa kujaza utupu wake na kumkamilisha. Si wawili tena bali sasa wamekuwa “mwili mmoja” (2:24). Hawajifuniki nguo na hawauonei haya “mwili mmoja” (2:24, 25). Hawana makovu ya kufichwa, hawana siri za kulindwa. Mapenzi ya ukaribu si haya! Nani aliyoyaanzisha mapenzi haya kama si Muumba aliyewaunganisha? Ukweli usioweza kufumbiwa macho ni huu: Mbunifu na Mjenzi wa mapenzi moto ni Mungu mwenyewe.
Tangia mwanzo “Mungu ni pendo” (1Yohana 4:8) na amebakia hivyo vizazi na vizazi. Hata baada ya Adamu na mkewe kumuasi Muumba wao, Mungu ameendelea kuonesha mapenzi yake ya wazi na karibu kwa watu wanaojificha na kukimbia mbali naye. Mapenzi yake kwa watu wake ni kama ya Bwana na bibi arusi wake na umoja wao, mmhhh, “siri hiyo ni kubwa [Τὸ μυστήριον τοῦτο μέγα ἐστίν·]” (Waefeso 5:32) huwezi kuanza kuijua mpaka uingie ndani.
Japo upendo wa Mungu kwa watu wake hauchunguziki (Warumi 11:33), upendo wake unafahamika kwa watu aliojifunua kwao. Gary Champan ametuonesha njia kadhaa ambazo Mungu anazitumia kufunua upendo wake kwa marafiki zake na ambazo tunaweza kuzitumia kuakisi upendo huo kwa wapenzi wetu.
Nikitambua bado mngali mkichumbiana, nitazijadili njia hizo kwa kiasi (nivumilie kama maji yatazidi unga). Huenda kiasi hicho cha maarifa kitakusaidia ujue namna ya kumleta mpenzi wako karibu yako huku mkisindikizana pole pole kuelekea madhabahuni ambapo mtatangazwa rasmi imekuwa “mwili mmoja.” na kupewa haki ya kupendana bila mipaka. Sasa una nafasi ya kutengeneza imara msingi wa ndoa yako, kwa kujifunza kumpenda mchumba wako kama Mungu anavyopenda marafiki zake wa karibu.
Picture
1. Mkaribie kwa maneno
Kwanza, Mungu anatumia maneno kutuonesha upendo unaotuleta karibu naye. Mungu anauzungusha ulimi wake na kudondosha maneno matamu yanayovutia usogee na kuyalamba.
Maneno ya kumthibitisha
Mungu anatuvuta kwa maneno ya kututhibitisha. Alipomposa kijana Yeremia awe nabii wake, Bwana Mungu alimwambia amemkubali kama yeye alivyo. Sikia Yeremia anavyokumbukia baadaye aliyoambiwa, “"Bwana alinitokea zamani, akisema, Naam nimekupenda kwa upendo wa milele,..." (Yer 31:3). Maneno ya uthibitisho kiasi gani! Ndiyo, maana Yeremia hakuweza kuyasahau! Unawezaje kusahau wakati umeambiwa unapendwa kwa upendo wa milele? Una wasi wasi gani wa kutelekezwa huku Mungu amekuthibitisha katika pendo kwa kukwambia, “sitakuacha kamwe, wala sitakutupa"? [tafsiri yangu](Waebrania 13:5)
Mshulami aliitumia lugha hii ya uthibitisho alipomkubali Sulemani kama wake binafsi aliposema “Mpendwa wangu ni wangu, na mimi ni wake" (Wimbo 2:16). Mtoto wa Daudi ajisikiaje kuambiwa hivyo?! Tafakari mvuto wa maneno yanayovuta moyo kama haya.
Fikiria maneno ya uthibitisho unayoweza kumtamkia mpenzi wako na kumfanya ajisikie amefika nyumbani awapo mbele zako. Mwambie: nakupenda, nakupenda milele. Usikariri; sema unapomaanisha. Hata akisikia “nakupenda” mara kwa mara hatachoka; ili mradi unamaanisha unachomwambia.
Unaweza kuwa mbunifu kwa kumwambia pia unamkumbuka, unamfurahia, unamheshimu, au vyovyote unavyomthamini jinsi alivyo. Kwamba ni mnyonge au ana nguvu, amekuudhi au amekufurahisha, ujumbe wako kwake uwe pale pale: ninakupenda ulivyo. Mthibitishe kwa maneno ya kumuonesha umemkumkubali kikamilifu.
Maneno ya kutia moyo
Mungu anapotuthibitisha anatujua hatukukamilika na ndiyo maana anatutamkia pia maneno ya kututia nguvu. Msikie anavyobembeleza wapenzi wake, “usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.” (Isaya 41:10). Mungu anaweza kutoa maneno hayo kwa kuwa anajua mizigo inayowalemea walala hoi. Waliochoka wanatiwa nguvu na maneno hayo kwa kuwa wanahisi Yuko anaowaaelewa na anataka kuwasaidia.
Huwezi kutoa maneno ya kumnyanyua aliyechoka kama ungali ukikalia kiti cha hukumu. Ukidhani mwenzio anajilegeza au anajiendekeza huwezi kumtia moyo. Lakini, unaposhuka chini usawa wa mwenzio alipo na kujaribu kuvaa kiatu chake na miwani yake, ndipo unapoweza kutazama ulimwengu kupitia macho yake na kuguswa na shida yake. Unapoguswa usisite kumtamkia. Mwambie: usijali, ninajua, tuko pamoja, ninaweza kukusaidia? Kuna hisia ya pekee moyoni unapotambua mwenzio anakuelewa unayopitia na bega lake ni imara kukutegemeza unapolegea.
Maneno ya kumsifia
Mungu haishii kuongea nasi maneno ya kutuhamasisha bali pia ya kutusifia. Nathanieli alipokutana na Yesu kwa mara ya kwanza, Yesu alimsifia mbele ya wenzake na kusema, “tazama, Mwisraeli kweli kweli, hamna hila ndani yake” (Yohana 1:47). Nathanieli akaruka kwa mshangao na kutaka kujua iweje ampongeze hivyo. Tokea hapo, Nathanieli akaandamana na Yesu kama mwanafunzi wake.
Maneno ya pongezi ukiyamtamkia kwa dhati yatamvuta mwenzio kuambatana nawe kama Nathanieli alivyovutwa kumfuata Yesu. Usiogope kumsifia kwa kuogopa utampoteza, eti utamtia kiburi. Pongezi za kweli zinagundisha wapendanao badala ya kuwaachanisha. Ukimpongeza kwa uzuri wake atakuwa radhi kukusikiliza unapomkosoa kwa ubaya wake.
Usichelewe, msifie. Bora kumsifia leo unapokuwa naye badala ya kumwagia sifa kesho unapomkosa (“lakini alikuwa mzuri”). Sulemani alipokuwa hai hakumficha Mshulami kumwambia uzuri wake. Alipomuimbia alisema, “Tazama, u mzuri, mpenzi wangu, U mzuri, macho yako…: Kama mpera kati ya miti ya msituni, Kadhalika mpendwa wangu kati ya vijana. (Wimbo 1:15; 2:13). Tunga shairi lako pia. Mfanye sasa ajisikie kuwa yeye ni wa pekee machoni pako. Mwache ajue urembo wa miguu yake mpaka fahari ya nywele zake ni vya thamani kwako, upole na ujasiri wake ni furaha yako. Usisubiri wenzako wamsifie kabla wewe haujamsifia. Msifie, usiibiwe. Mvute mpenzi wako kwako kwa kamba za sifa, uone kama hajakusogelea kwa karibu zaidi.
2. Mkaribie kwa vitendo
Zaidi ya maneno, Mungu hupenda kwa vitendo. Matendo huongea kwa sauti kubwa kuliko maneno. Ukinipenda kwa vitendo unanifanya niamini maneno yako. Matendo ya msaada ni mapenzi yaliyochukua maumbile halisi. Unaweza kutilia mashaka maneno yasiyoshikika, lakini si matendo yanayokugusa moja kwa moja. Anayependa hata kujitoa kumsaidia mpendwa anajua kupenda kuliko wengine wote. “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.” (Yohana 15:13)
Mpenzi asipokuwa hatarini kufa, upendo hautakusukuma kuutoa uhai wako kwa ajili yake. Lakini utakubidisha kumsaidia kila inapobidi. Unapomsaidia umetoa sehemu ya uhai wako kwa manufaa yake. Kwa pesa zako, kwa nguvu zako, kwa akili zako, kwa namna yoyote, msaidie apate kujua unampenda. “Katika hili tumelifahamu pendo, kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu. (1Yoh 3:16)”
Msaada upi unastahili kumpa? Msaada wowote utakaokidhi hitaji lililopo. Geuza macho yako. Mwangalie mhitaji na usijiangalie mtoaji. Kama anahitaji umsindikize hospitali na wewe unamkodishia taxi utakuwa kama shirika la misaada linalowaletea wanakijiji mitumba huku maji safi na salama ndiyo hitaji lao. Atakushukuru, lakini atahisi umempuuza. Mwangalie yeye anahitaji nini na si jamii itasemaje. Utamaduni na malezi ya nyumbani yakikuzuia kumpa msaada anaouhitaji, mwenzako atahisi unapenda kabila lako kuliko yeye. “Katika hili tumelifahamu pendo, kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu. (1Yoh 3:16)”. Unakumbuka mpenzi wako amelalamika anahitaji nini? Tafuta namna umsaidie. Utakapojaribu kuvaa kiatu cha mwenzako na kuhisi mwiba unaomsumbua hautasita kumuonesha unampenda kwa kumsaidia inavyohitajika.
Uvaapo mwilini sura ya upole na uelewa na utayari wa kusaidia, mwenzako hataogopa kukuomba msaada anaouhitaji. Mshulami anapokutana na mchumba wake Sulemani waliopotezana hasiti kumwambia shida inayomsumbua kichwani. Anamwambia, “tukamatie mbweha, Wale mbweha wadogo, Waiharibuo mizabibu, Maana mizabibu yetu yachanua.” (Wimbo Ulio Bora 2:15)
Picture
3. Mkaribie kwa muda
Mungu aliwapenda wanawe aliowaumba hata akatenga muda wa kuwa nao. Ilikuwa kawaida yake kuwatembelea Adamu na Hawa na wazazi wetu hata waliweza kutofautisha mwendo wa Tembo na wa Mungu bustanini. Siku walipojificha baada ya kula tunda walilokatazwa, “wakasikia sauti ya Bwana Mungu, akitembea bustanini wakati wa jua kupunga” (Mwanzo 3:8). Zaidi ya matembezo hayo, Mungu alitenga siku moja katika juma ya kupumzika na kustarehe pamoja na wanawe (Mwanzo 2:1-3). Familia iliyo pamoja hutenga muda wa kutumia pamoja, usioingiliwa na shughuli zinazowatenga.
Hata wachumba wanaokusudia kujenga familia inayothamini muda wa pamoja watajali faragha ya wakati wao. Mshulami anakumbukia jinsi Sulemani alivyomuite wakatoke kwani wakati umewadia:
Mpendwa wangu alinena, akaniambia,
Ondoka, mpenzi wangu, mzuri wangu, uje zako,
Maana tazama, kaskazi imepita, Masika imekwisha, imekwenda zake;
Maua yatokea katika nchi, Wakati wa kupelea umefika,
Na sauti ya mwigo husikiwa kwetu.
Mtini wapevusha tini zake, Na mizabibu inachanua, Inatoa harufu yake nzuri;
Ondoka, mpenzi wangu, mzuri wangu, uje zako.” (Wimbo Ulio Bora 3:10-13)
Ungetamani mngetoka na mwenzako kwenda mandhari kama haya? Huitaji kwenda mashariki ya kati au Parisi kufurahia muda wenu wa pamoja. Waweza kumchukua kwenye mgahawa wa heshima kwa chakula cha mchana au kutembea pembezoni mwa bahari pamoja au kuangalia movie pamoja au someni kitabu pamoja au fanyeni mazoezi pamoja au kulima bustani pamoja. Tumieni muda pamoja kuongelea maswala yanayowahusu na kwa kina kirefu. Mazingira yoyote huru na salama yatawapa muda mnaouhitaji. Mkiutumia vizuri utengano wa kutofahamiana kati yenu utazidi kupungua siku kwa siku.
4. Mkaribie kwa zawadi
Watu wamekua wakimkaribia Mungu kwa sadaka na dhabihu mikononi lakini Mungu anawajia kwa kujitoa mwenyewe katika Mwana wake kama sadaka (Yohana 3:16). Upendo ni chemchem inayotoa na kupokea maji. Endapo unatoa bila kupokea au unapokea bila kupokea upendo utakauka. Baada ya Mungu kumpatia Ibrahimu sadaka ya mtoto, baadaye akamwambia amrudishie kama sadaka (zawadi). Ibrahimu alipojaribu kumtolea Mungu Isaka kama zawadi, ndipo malaika wa Bwana akamwambia, “sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee.” (Mwanzo 22:12). Baada ya hapo Mungu akathibitisha upya agano la mahusiano yake naye.
Kama ilivyo kawaida, wapenzi walio karibu hupeana zawadi. Mshulami akiangalia mashavu ya Sulemani anasema ni mazuri kwa mashada na shingo yake kwa mikufu ya vito. Halafu anasema, “Tutakufanyizia mashada ya dhahabu, Yenye vifungo vya fedha.” (Wimbo 1:11). Mfalme Sulemani anaweza kujipamba, ana dhahabu na fedha, lakini mapambo kutoka kwa mpenzi wake ni ishara ya upendo.
Pokea zawadi kutoka kwa mwenzako kama lugha ya upendo. Anapokupatia anakwambia, “nilikufikiria.” Alikufikiria vya kutosha kiasi cha kutaka ujue uko mawazoni mwake. Haijalishi zawadi kubwa au ndogo lakini kama inaonesha alikufikiria ipokee kwa furaha. Zawadi iliyopokelewa ina mguso wa pekee kwa mtoaji. Ukipokea ataguswa kukuzawadia tena na tena ili kukufurahisha.
Japo zawadi ni zawadi tu, zawadi inayoonesha mtoaji aligharimika kufikiri na kujiuliza “nitamfurahishaje?” ndiyo zawadi yenye thamani. Si lazima iwe ya bei lakini yapaswa ionekane ya thamani machoni kwa mtoaji na mpokeaji. Zawadi isiyomgharimu mtoaji fikara au muda si zawadi anayostahili mpendwa wa roho.
Zawadi ya thamani kuu kwa wapendanao ni uwepo binafsi wa mpenzi kwa mwenzake. Haijalishi unatoa zawadi nono kiasi gani, lakini kama haupatikani anapokuhitaji zawadi unazomletea zinapungua uthamani wake. Wapenzi wanathamini uwepo wa mpenzi pembeni yao kuliko vitu. Ni kama mtoto aliyemkosa baba aliyepotea nyumbani kwa miezi kadhaa. Baba anaporudi ni mikono iliyojaa zawadi, mtoto anamkumbatia baba asimuachie na kumwambia “ulikuwa wapi?” Hazioni zawadi anamuona baba zaidi. Zaidi ya simu na nguo na viatu na vitu vingine vyovyote, mpe mwenzako uwepo wako na hasa anapokuhitaji.
Picture
5. Mkaribie kwa mguso
Mungu anagusa watu
Kwa kugusa Mungu anaonesha jinsi anavyotupenda kwa karibu. Tofauti na viumbe vyote alivyoviumba, Muumba alipomuumba mwanadamu kwa mikono yake alimbusu kwa kumwekea mdomo puani na kumpulizia pumzi ya uhai (Mwanzo 2:7). Yesu Kristo kwa mguso alimponya mtu asiyeguswa na yeyote kwa sababu ya uchafu wa ukoma wake. Angeweza kuishia kumwambia, “Nataka, takasika,” na angepona. Lakini akaenda maili ya pili kumgusa. Kwa kumgusa alikuwa anamwambia siko mbali nawe. Wanafunzi walipoogopa sana baada ya Yesu kuwabadilikia sura yake na kung’aa kama jua, aliwagusa na kuwaambia wasiogope (Mathayo 17:7). Kwa kugusa watu Yesu alikuwa ninawapenda kwa ukaribu huu.
Pia, Yesu alikubali kuguswa kama ishara ya upendo wa karibu. Mwanamke “aliyekuwa mwenye dhambi” na “aliyesamehewa sana” hakujua njia bora ya kumrudishia upendo Yesu zaidi ya kumbusu. “Akasimama nyuma karibu na miguu yake, akilia, akaanza kumdondoshea miguu machozi yake, na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake, akiibusu-busu miguu yake na kuipaka yale marhamu” (Luka 7:38). Yesu akakubali busu kama ishara ya upendo wa karibu mwanamke aliokua nao kwake (fungu 47)
Mama anagusa mwanawe
Kila mtoto anahitaji upendo na kila mtoto anahitaji mguso wa mama. Matabibu wamethibitisha kwamba mtoto asiyenyonya kwa mama, asiyekumbatiwa, anayeshinda mwenyewe na kulala kitandani pekee yake, afya yake inadhurika na ukuaji wake unaathirika. Yesu akijua hitaji la watoto kuguswa, aliwaruhusu waje kwake ili awaguse (). Si vema kwa mtoto au mseja kukaa pekee yake pasipo kuguswa ngozi. Ngozi ni ganda linalofunika yote yaliyomo ndani yake. Ukigusa ngozi umegusa roho iliyoko ndani yake.
Mpenzi anamgusa mwenzake
Siyo siri: mguso unagusa roho na hasa unapotoka kwa mpenzi wa rohoni. Malikia Mshulani anatambua utamu huo anapomtamkia mpenzi wake, “Kubusu na anibusu kwa kinywa chake. Maana pambaja zako zapita divai” (Wimbo 1:2). Mshulami hajarukwa na akili anapotamani busu; isipokuwa ni mpenzi wa kawaida katika mahaba ya kawaida.
Mguso stahiki sio tu jambo linalotazamiwa na wapendanao bali ni njia ya muhimu ya kuoneshana uhusiano wao umekua kwa masafa yapi. Wapenzi walio katika uchumba hawatagusana mpaka kileleni kama wako kwenye ndoa. Marafiki waliofahamiana wiki mbili zilizopita hawatapapasana kimapesi kama wachumba wa miezi tisa. Vigezo na masharti yazingatiwe. Hisia za mapenzi sharti zisichochewa kabla ya wakati; hazina budi kuachiwa kukua kuendana na uhusiano uliopo. “Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, Hata yatakapoona vema yenyewe” (Wimbo 2:7). Ni akina nani wanaochochea mapenzi kabla ya wakati?
Wapenzi “wanaochochea mapenzi”
Wanaowahi mno kuchochea mapenzi kabla ya wakati ni wale wanaoingia katika uhusiano wa karibu pasipo kujitambua.
Binti asiyejitambua anadhani anaposhikwa-shikwa anapendwa na kumbe mwenzake anataka tu amtumie kutuliza tamaa yake. Huko nyumbani alikua kivyake na alikosa kuguswa, kushikwa, kukumbatiwa; sasa anapoguswa na mpenzi anadhani anapokea upendo alioukosa. Bila kujitambua anamruhusu aendelee kumgusa hata hawezi kumwambia hapana tena. Badala ya kujitambua kama binti wa Mungu anayependwa sasa anajitambua kuwa mateka wa mahaba anayeburutwa sana. Si moto huo?!
Kijana asiyejitambua sawa anapompapasa binti ndipo anaamini kumbe sasa yeye ni mwanamume. Anatafsiri uanaume wake kwa ushawishi wake. Kama akimgusa zaidi na mwenzake akamfurahia zaidi basi ni mwanamume zaidi. Kama asipozuiwa ataendelea kupapasa na kupapasa (sijui anatafuta nini..hahaha) tena na tena mpaka anafika umbali ambao hawezi kurudi nyuma. Mwishoni, badala ya kujitambua kama mtoto wa Mungu aliyekamilika sasa anajihisi amekua mtu mtumwa wa tamaa zake mwenyewe. Kijana amekanyaga moto!
Vile vile wanaochochea mapenzi kabla ya wakati ni wale wanaoingia katika mapenzi pasipo kutambua uwezo wa mahaba.
Wanadharau kwamba “Upendo una nguvu kama mauti…mwako wake ni mwako wa moto” (Wimbo 8:6). Hawajali moto na kuusogelea. Wanapenda kukaa wenyewe sirini kuliko hadharani. Wakiwa wenyewe faraghani hawana breki, hawana kiasi na wanapenda kupapasana kuliko kuongea. Badala ya kuuota moto kwa mbali, wanachagua kuukaribia. Mwishoni moto unawateketeza. Wanaingia kwenye ndoa kabla ya wakati. Wanadhani wamefahamiana vya kutosha kumbe wamesisimuana vya kutosha.
Tena wapenzi wanaochochea mapenzi kabla ya wakati ni matapeli walio na nia ya kuingia katika uhusiano kwa lengo la uharibifu tu; yaani, kufanya mapenzi haramu.
Wako radhi kupita njia yoyote ili mradi inawaongoza Rumi. Hawahitaji kukupapasa ngozi ili kutimiza malengo yao. Hutumia hata macho yao kama nyezo ya kukuamsha ashiki ili uzini naye. Yesu amemaliza yote aliposema, “Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.” (Mathayo 5:28). Kwa kuwa moyoni wamedhamiria kuzini, hawajui kumtazama mpenzi kama mtu wa kuheshimiwa, isipokua kama kipozeo cha tamaa zao chafu. Utajuaje kuwa mpenzi wako anasukumwa na tamaa chafu?
Tambua miguso ya “uchochezi”
Miti yote ni miti, tofauti yake ni matunda yake. Miguso yote ni miguso lakini ya uchochezi inajulikana kwa matunda yake. Kama mpenzi wako anasukumwa na tamaa chafu utamtambua kwa kutazama matendo yake.
Kama mtu mwenye njaa anavyoongelea chakula tu, mazungumzo yake yatakua yanaelekea kwenye mapenzi ya kimwili tu (kana kwamba hakuna mada nyingine). Tena kama atapata nafasi hataweza heshimu msimamo wako. Atahangaika kukurubuni au kukusukuma ulegeze msimamo. Usidanganyike, tamaa haina subira lakini upendo “huvumilia” (1Wakorinto 13:4). Tamaa haijui heshima; lakini upendo “haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake“ (fungu, 5). Usisahau, mtu anayesahau kuwa ipo shule ya kumalizwa na upo msingi wa kujengwa na yapo malengo yakufikiwa na yapo majina ya kulindwa, na yupo Mungu wa kuogopwa, huyo anatafuta kutimiza tamaa yake tu na si mahitaji yako.
Furahia miguso salama
Japokuwa ipo miguso ya uchochezi yenye matokeo mabaya, haimaanishi haipo mizuri. Usiache kufurahia mihogo salama kwa sababu umeambiwa ipo yenye sumu. Sumu ni moyo mchafu. Kama hamna nia mbaya, mwaweza kutembea mmeshikana mikono, mkakaa benchi moja, mkagusana miguu mkiwa mezani, mkalishana chakula au vinginevyo kutegemea na umbali mlioufikia katika safari yenu ya kukaribiana. Msalimie mpenzi wako kwa mkono mzima. Ukimpa nusu, umempunja penzi. Mkikutana mkumbatie au mbusu kuonesha umefurahia kumuona.
Mwaweza kufanya hayo na mengineyo kama mazingira yanawaruhusu. Inaweza isiwape ninyi shida, lakini wanaowatazama wakaudhika. Mshulami alitambua watu wa jamii yake wasingeona vibaya kumuona anambusu mdogo wake wa kiume hadharani; lakini wasingemuelewa ambusu mchumba wake mbele yao. Akamwambia Sulemani, “laiti ungekuwa kama ndugu yangu, Aliyeyanyonya matiti ya mamangu! Kama ningekukuta huko nje, Ningekubusu, asinidharau mtu. (Wimbo 1:2; 8:1)”. Busara ndiyo kiongozi wa mapenzi salama.
Lakini busara isiyo na ujasiri ni woga katika vazi la hekima. Msishindwe kuoneshana upendo kwa sababu ya kuogopa jamii (mkiendelea hivyo, baadaye katika ndoa mtashindwa kusaidiana kazi kama kuosha nguo kwa sababu ya kuogopa kuvunja tamaduni). Jizuieni kukaribiana hadharani; ikiwa kwa kujizuia, Mungu atatukuzwa na jamii bora itajengwa (1Wakorinto 10:31). Lakini msinyimane upendo wa mguso kwa sababu tu mnaogopa mtasemwa msijechafuliwa majina. Swala si kulinda majina; isipokuwa majina yapi ya kulindwa. Kumbukeni kuwa ninyi si watumwa bali wana. Mlipompokea Yesu na kufanywa wana wa Mungu “hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba.” (Warumi 8:15)
Picture
Mwisho
Wachumba waliofanyika wana na binti wa Mungu ndiyo wanaoweza kupendana kwa dhati. Hamuwezi kuiga upendo wa Mungu; mnapaswa kuzaliwa naye. Mungu awamwagie pendo lake moyoni mwenu na penzi lenu lijae na kuwabubujikia katika kuwaburudisha daima. Mahusiano ni matamu, maisha yana raha, panapokuwepo upendo wa kweli, wa dhati, na wa karibu.
Huenda kama umekua katika uhusiano wa kawaida, sasa unahamu ya kuingia kwenye mapenzi ya karibu na mwenzako. Kabla ya kufanya hivyo ni muhimu ujibu maswali makuu manne yatakayokujulisha kama upo tayari au la. Kila mtu anahitaji mapenzi hayo lakini si kila mpenzi aliye tayari.
Nikikurudia, tutaongelea zaidi hayo. Mungu awabariki.
from SMS ZA MAHABA https://ift.tt/3IgIVMz