TABIA 8 ZA WAPENZI WENYE PENDO LA DHATI.

 



MAPENZI ni hisia. Unapompata mtu akakupenda kwa dhati, ni vigumu sana kuyatambua mateso ya wengine wanayopitia kwenye mahusiano yao. Wapendanao wanajiona wapo kwenye dunia yao, wanapokuwa pamoja wanajihisi matajiri hata kama ni kapuku. 

 


Unapokosea kumchagua mwenzi wa maisha mara nyingi unajikuta kwenye mateso mazito na siku zote kati ya mtihani mgumu kuufaulu katika masuala ya uhusiano wa kimapenzi ni kumpata mwenza sahihi mwenye mapenzi ya dhati.

 

Wengi wamejikuta wakiingia kwenye uhusiano na watu ambao hawana mapenzi ya dhati. Wanateseka, wanajaribu kuwavumilia wenzi wao ili labda pengine wanaweza kubadilika lakini wapi. Mwisho wa siku wanaishia kuachana. Ni vizuri sana kwa wale wanaokwenda kuanzisha mahusiano mapya, wakawa makini sana katika kufanya utafiti juu ya wenza wao. Jiulize, unayempenda ana mapenzi ya dhati? Atakujali? Atakuthamini? Atakupa kipaumbele? Atakuheshimu?

 

Hili linawezekana endapo tu utafanya uchunguzi mapema kwa wakati ule unaoanzisha uhusiano. Mwenye upendo wa dhati utamjua tu endapo utakuwa makini. Penzi la kweli halilazimishwi, linaonekana dhahiri shahiri. Mpenzi wako unamjua kama ana mapenzi ya dhati kwako hata kwa kumuangalia tu machoni, anavyokujali, anavyokuhitaji na hata jinsi anavyokuthamini.

 

Ili kupata picha ya watu wanaopendana kwa dhati, leo tuziangalie tabia 8 za watu ambao wanapenda kwa dhati. Ukiona tabia hizi nane hazipo kwenye uhusiano wako basi ujue kabisa haupo kwenye uhusiano ule ninaouita wa dhati, uhusiano ambao unawafanya muishi kwenye dunia ya peke yenu:

 

KUJUANA

Wenye mapenzi ya dhati huwa wanajuana hali zao. Mwanaume anamjua vizuri mwenza wake kwamba yupo katika hali gani. Ana furaha au huzuni? Ana mawazo au anaumwa bila hata ya kuambiwa anakuwa ameshamjua mwenzi wake.

MAPENZI SIO KIPAUMBELE

Wanaopendana kwa dhati hawakamilishi uhusiano wao kwa tendo la ndoa tu pekee bali kuna mambo mengi wanayofanyiana nje ya kufanya tendo hilo. Wataalam wa masuala ya mahusiano wanasema tendo la ndoa ni moja ya sehemu kati ya vitu mia moja vinavyofanywa na wapendanao kukamilisha uhusiano.

 

KUTANIANA

Wenye mapenzi ya dhati wana ‘kautani kao ka kimapenzi.’ Hako kautani kao ni ka-ndani na wanakaelewa wao wenyewe, yawezekana mtu wa nje asiweze kabisa kukabaini.

 

KIPAUMBELE

Wenye mapenzi ya dhati wanapeana kipaumbele. Kila mmoja anampa kipaumbele mwenzake kuliko kitu kingine chochote, hayo ndio mapenzi ya dhati.

 

KUAMINIANA

Tabia ya watu wanaopendana kwa dhati pia huwa wanakuwa wanaaminiana. Kila mtu anamuamini mwenzake na kila mmoja anayeaminiwa anajiheshimu na kuilinda heshima yake.

 

HAWAFICHANI

Wapendanao ambao wanaishi kwenye dunia ya kupendana kwa dhati mara nyingi si watu wa kufichana. Wanaelezana ukweli, wapo huru kusema ukweli kuliko kusema uongo.

WANAZUNGUMZA LUGHA MOJA

Wanaopendana kwa dhati wanazungumza lugha moja katika masuala mbalimbali yanayowahusu. Utadhani wanawaza pamoja kumbe wapi, wanashibana na mambo yao huandika kumbukumbu ya pamoja kutokana na utu, kujaliana na kuheshimiana.

 

WANASHIBANA TENDO

Wapendanao wenye mapenzi ya dhati wanashibana tendo. Wanajuana miili yao, kila mmoja anaujua vizuri mwili wa mwenzi wake hivyo wanalifanya tendo la ndoa kuwa kwenye kiwango cha juu pindi wanapolifanya. Kwa leo naishia hapa. Tukutane wiki ijayo, unaweza kunifuata kwenye mitandao yangu ya kijamii. Instagram na Facebook natumia Erick Evarist, Twitter natumia ENangale



from SMS ZA MAHABA https://ift.tt/3AeTlqK

Post a Comment

Previous Post Next Post